MANCHESTER United imepata pigo kubwa baada ya straika wake
mahiri Robin van Persie kuumia paja na kwamba atakuwa nje ya uwanja kwa
mwezi mmoja.
Fowadi huyo wa Uholanzi aliumia wakati akipiga
kona iliyosababisha bao la Manchester United kwenye mechi ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya dhidi ya Shakhtar Donetsk Jumanne iliyopita na sasa
majeraha hayo yatamweka nje ya uwanja hadi mwakani.
Majeraha hayo ni pigo kubwa kwa kocha David Moyes
ambaye kwa sasa anahaha kuinusuru Manchester United kukwepa kipigo cha
tatu mfululizo kwenye Ligi Kuu England wakati itakapomenyana na Aston
Villa kesho Jumapili.
Van Persie atakosa mechi nane za mabingwa hao wa England ukianzia Aston Villa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Villa Park.
Moyes alisema: “Robin amepata majeraha ya paja na
atakuwa nje kwa mwezi mmoja. Alikuwa anapiga kona dhidi ya Shakhtar na
hapo alijiumiza paja. Tutamkosa tena Robin, safari hii kwa mwezi mzima.”
Mechi atakazikosa Van Persie ni dhidi ya Aston
Villa, Stoke City, West Ham United, Hull City, Norwich City, Tottenham
Hotspur na Swansea City mara mbili kwenye Ligi Kuu na Kombe la FA.
No comments:
Post a Comment