![]() | |
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic ameeleza kuwa kuna mambo mengi yanayotakiwa kufanyiwa kazi katika kikosi cha Simba ili timu ifanikiwe na jambo la kwanza aliloona halijakaa sawa ni mishahara ya wachezaji |
MCHUJO wa wachezaji wa Simba unaodaiwa
kutangazwa na Kocha Zdravko Logarusic umezua zogo Simba kwani viongozi
walitarajia kukutana naye haraka ili kufahamu vigezo vilivyotumika
katika mchakato huo.
Inadaiwa Logarusic ametangaza wachezaji 26 wa
kuendelea na Simba huku wengine sita wakitemwa kwa madai ya kutohitajika
kikosini na kutakiwa kwenda kikosi B.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Simba, Danny
Manembe ameliambia Mwanaspoti kuwa hadi jana Jumatatu mchana majina hayo
yalikuwa hayajafika mikononi mwao kwa kuyathibitisha kwani walipanga
kufanya kikao na kocha huyo jioni ili kuyajadili.
“Hayo majina sijajua yametoka wapi maana kocha
hawezi kuacha au kuwashusha wachezaji kutoka kikosi cha kwanza bila ya
sisi watu wa ufundi kufahamu, tunakutana naye leo (jana Jumatatu) jioni
na kuyapitia majina ya wachezaji anaodhani anataka kubaki nao kikosini
au kuwatema.
“Tutatazama vigezo vilivyotumika na kama
tukiridhishwa navyo tutapitisha maana mchezaji mwingine anaweza kukataa
kucheza kwa mkopo au kwenda timu B kulingana na mkataba wake,” alisema
Manembe.
Aliongeza: “Pia inawezekana kocha akaamua
kuwapunguza aliowapunguza lakini akawa hayuko sahihi maana kuna
wachezaji wametajwa kupunguzwa lakini hata mazoezini hawakufika hata
mara moja, sasa labda tukutane naye tujue katumia vigezo gani kuwaacha.”
Baadhi ya wachezaji waliotajwa kuenguliwa kikosi
cha kwanza ni Andrew Ntalla, Sino Augustino na Ibrahim Twaha ‘Messi’
Marceil Kapama, Rashid Ismail na Adeyun Seif.
Waliobaki ni Yaw Berko, Abuu Hashim, Omary Salum,
Haruna Shamte, Issa Rashid, Said Nassor ‘Chollo’, Hassan Khatib, Joseph
Owino, Miraji Adam, Gilbert Kaze, Said Ndemla, Jonas Mkude, Henry
Joseph, William Lucian, Abdulhalim Humud, Ramadhan Singano, Ramadhan
Chombo, Amri Kiemba, Uhuru Seleman, Haruna Chanongo, Amis Tambwe, Badru
Ally, Edward Christopher, Awadhi Juma na Betram Mwombeki.
Kwa upande wake Sino aliiambia Mwanaspoti kuwa
yupo tayari kwenda kucheza popote kwa mkopo kwani anaamini yanayotokea
si maamuzi ya kocha.
“Kabla hata kocha hajafika niliambiwa na kiongozi
mmoja kwamba, natakiwa kwenda kucheza kwa mkopo JKT Ruvu bila ya
kufafanuliwa zaidi, sasa niliposikia haya nikaona ndiyo yale yale. Mimi
ni mchezaji najiamini katika uwezo wangu na nitacheza popote pale.
“Mimi naamini kuna watu wameamua kumpa kocha
majina haya na yaliandaliwa hata kabla hajafika.Wengine hawapo katika
timu wameachwa, wengine wamebakizwa sasa kigezo kipi kimetumika,”
alisema Sino.
Twaha ambaye anafahamika pia kama Messi,
alisajiliwa Simba msimu huu akitokea Coastal Union alisema; “Mimi naumwa
tangu Oktoba 10 nilipochanika nyama za paja, sasa naachwa kwa kigezo
kipi? Labda kwa kuumwa, hata kama napelekwa kwa mkopo au timu B
nitatumikia vipi?” Alihoji mchezaji huyo.
No comments:
Post a Comment