![]() |
Kipa,Juma Kaseja.
|
KIPA,Juma Kaseja, juzi Jumamosi aliichezea Yanga mechi yake ya kwanza baada ya kurejea klabuni hapo hivi karibuni akitokea Simba na kudaka mashuti 17 katika dakika 90 za mchezo wa kirafiki dhidi ya KMKM ya Zanzibar. Mechi ilimalizika kwa Yanga kushinda mabao 3-2.
Kaseja ambaye aliwahi kuidakia Yanga kwa msimu
mmoja 2009/2010, alirejea mwezi uliopita kwa mkataba wa miaka miwili
baada ya kuachwa na Simba kabla ya kuanza msimu huu.
Mashabiki wa Yanga walipiga makofi ya kuashiria
kumkubali Kaseja wakati timu zikiingia uwanjani naye aliwajibu kwa
kuwanyooshea mikono.
Kaseja aligusa mpira kwa mara ya kwanza dakika ya
sita baada ya kurudishiwa na beki wa kati, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
kisha akampasia Juma Abdul.
Katika kipindi cha kwanza Kaseja alidaka mashuti
tisa yaliyoelekezwa langoni kwake na washambuliaji wa KMKM akina Ali
Shiboli, Ibrahim Hamis na Haji Simba.
Hata hivyo, Kaseja alifungwa mabao mawili dakika
za 69 na 72 wafungaji wakiwa ni Simba na Shiboli ambao walitumia vyema
makosa ya mabeki wa Yanga waliojichanganya kuokoa hasa baada ya
Cannavaro kutolewa dakika ya 65 na nafasi yake kuchukuliwa na Rajab
Zahir.
Katika kipindi cha pili, Kaseja alidaka mashuti
manane na kufanikiwa kupangua mipira miwili na kuifanya kuwa kona ambazo
hazikuzaa matunda.
Mara baada ya mchezo huo, Kaseja aliliambia
Mwanaspoti kwamba amefurahi kucheza mechi ya kwanza Yanga na kufanya
vizuri licha ya kufungwa mabao mawili.
“Naona nimeanza vizuri na yaliyotokea ni mambo ya
kimchezo tu, ninauamini ukuta wa Yanga na nadhani makosa yaliyojitokeza
tutayarekebisha kwa kushirikiana na kocha,” alisema
No comments:
Post a Comment