Tuesday, 10 December 2013

KOSTA PAPIC AMCHARUKIA KASEJA YANGA


Kocha wa zamani wa Yanga, Kosta Papic  

KOCHA wa zamani wa Yanga, Kosta Papic amemponda Juma Kaseja kwa kujiunga na klabu hiyo ya Jangwani na kumuita kigeugeu.
Papic, ambaye sasa ni Kocha Mkuu wa Black Leopards ya Afrika Kusini inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, alisema alichokifanya Kaseja ni kukosa msimamo.
Kocha huyo wa Serbia alifafanua kuwa Kaseja aliwahi kusajiliwa Yanga na kudumu nayo msimu mmoja wa 2008/09 kabla ya kuondoka baada ya pande zote mbili kutoridhika.
“Alipokuwa Yanga aliondoka baada ya msimu mmoja na alisema kuwa hakufurahia maisha ya Jangwani, sasa ni lini ameona maisha ya huko yamekuwa mazuri, binafsi nadhani amekosea, hakustahili kwenda sehemu ambayo amewahi kusema hana furaha,” alisema Papic, ambaye alijiunga Yanga wakati Kaseja akiwa amerejea Simba.
Huku akimponda Kaseja kwa kujiunga na Yanga, Papic amemsifu Yaw Berko kwa kujiunga na Simba na kusema atawasaidia sana.
“Huyo Berko nakubaliana naye kwa sababu Yanga walimuacha na kumuona hafai, lakini naye kama angekuwa amewahi kuchezea Simba nisingekubaliana naye, ila kwa sababu anajiunga nayo kwa mara ya kwanza nasema atawasaidia sana Simba,” alisema Papic alipozungumza na Mwanaspoti kutoka Polokwane, Afrika Kusini.
Papic ndiye aliyesamsajili Berko msimu wa 2009/10 baada ya kumtoa katika klabu ya Liberty Professionals ya Ghana ambako yeye alikuwa kocha wa Hearts of Oak ya mjini Accra.
Papic amewahi kufundisha Kaizer Chiefs, Maritzburg United, Orlando Pirates za Afrika Kusini ; Lobi Stars, Enyimba, Enugu Rangers na Kwara United za Nigeria.
Desemba 2008 alikwenda Ghana ambako alijiunga na Heart of Oak mpaka Julai 2009 alipoondoka na kujiunga na Yanga ya Dar es Salaam kwa vipindi viwili tofauti.



No comments:

Post a Comment