
Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting,Charles Boniface Mkwasa.PICHA|MAKTABA
KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Boniface
Mkwasa, ameweka wazi kwamba yupo katika mazungumzo na viongozi wa Yanga
na yakikamilika atatua Jangwani kuchukua nafasi ya Kocha Msaidizi,
lakini kiraka Mbuyu Twite ametoa masharti ya mkataba mpya.
Mkwasa ambaye aliwahi kuitumikia Yanga miaka ya
nyuma akiwa mchezaji na hata kocha mkuu, amesema alifuatwa na mabosi wa
klabu hiyo ambao tayari mazungumzo yao yamefikia sehemu nzuri, lakini
akagoma kuweka bayana alichozungumza nao.
Ujio wa Mkwasa umekuja baada ya Yanga kumpa notisi
ya siku 30 Kocha Mkuu, Ernest Brandts, huku fagio kubwa likitarajiwa
kupita kwenye vichwa vilivyosalia katika benchi la ufundi alipo Kocha
Msaidizi, Fred Minziro.
Mkwasa amesema mabosi hao wa Yanga katika
mazungumzo aliyofanya nao, wameonyesha nia ya kumrudisha kuwa kocha
msaidizi ambapo kocha mkuu atakayechukua nafasi ya Brandts bado
hajajulikana.
“Nikweli nimefanya mazungumzo na viongozi wa
Yanga, wanaonyesha wanataka kunipa nafasi ya kocha msaidizi, mazungumzo
bado yanaendelea hatujafikia mwisho katika kujua nini tumekubaliana,”
alisema Mkwasa.
“Mimi nipo tayari kurudi Yanga, lakini kwa sasa
siwezi kukuhakikishia kuwa nimepewa nafasi hiyo, ningekuomba usubiri
viongozi wa klabu ndiyo watakupa jibu la moja kwa moja, hakuna haja ya
kuwa na haraka katika hilo.”
Endapo Mkwasa atapewa nafasi hiyo, ni wazi kuwa
itakuwa ni kwaheri kwa Minziro ambaye kila mara Yanga inapokuwa kwenye
matatizo huitwa kuokoa jahazi kwa vile ni mwanachama na mchezaji wa
zamani wa timu hiyo.
Katika hatua nyingine, wakati wachezaji muhimu wa
Yanga wakiongeza mikataba yao klabuni hapo, beki kiraka, Mbuyu Twite,
amegoma kusaini mkataba mpya akitoa sharti kwamba asubiriwe mpaka msimu
umalizike.
Kwa mujibu wa kanuni za soka za kimataifa, beki
huyo yupo huru kufanya mazungumzo na klabu yoyote kwa ajili ya kuichezea
kutokana na mkataba wake kubakisha miezi mitano.
Akizungumza na Mwanaspoti, Twite alisema: “Najua
kama mkataba wangu unamalizika mwishoni mwa msimu huu wa ligi, wapo
baadhi ya wachezaji wameongeza mikataba mingine mipya, lakini kwangu
bado kwanza nasubiria ligi imalizike ndiyo nisaini mkataba mwingine mpya
kama tutaafikiana kwa vile mimi naangalia fedha.
“Nimeanza kufanya mazungumzo na viongozi kwa ajili
ya kusaini, nimewaambia wasubiri kwanza ligi imalizike ndiyo niaamue.
Ninajua zipo timu zitanifuata kwa ajili ya kunisajili, lakini kwanza
nitaipa nafasi timu yangu ya Yanga kwa kuangalia ofa yao watakayonipa
kabla ya sijachukua uamuzi mwingine.”
Kocha aliyeondoka Azam, Stewart Hall, alikuwa
amepanga kumsajili beki huyo baada ya mkataba wake kumalizika na Yanga.
Habari za ndani zinadai kwamba beki huyo anasusa kusajili kwa vile
lolote linaweza kutokea na akapata dau kubwa kutoka kwa mahasimu wa
Yanga.
No comments:
Post a Comment