Thursday, 12 December 2013

OKWI, MAFISANGO WANA SIRI YA MANJI

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji 


INAFAHAMIKA kuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, ametangaza kutogombea katika uchaguzi ujao wa klabu hiyo, lakini unafahamu kilichomfanya akaamua kugombea uenyekiti katika uchaguzi mdogo ule wa Julai mwaka jana? Mwenyewe anasema ni kipigo cha 5-0 walichopewa na Simba.
Yanga ilikumbana na kipigo hicho Mei 6 mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo wafungaji wa Simba walikuwa; Emmanuel Okwi (mawili), Felix Sunzu, Juma Kaseja na Patrick Mafisango (marehemu sasa).
Wakati huo Yanga ilikuwa katika mgogoro wa uongozi na aliyekuwa Mwenyekiti, Lloyd Nchunga, akalazimika kuachia ngazi ndipo Manji alipochaguliwa miezi miwili baadaye katika uchaguzi uliofanyikia Diamond Jubilee na kushinda kwa asilimia 97 ya kura.
“Niliamua kuwania uongozi Yanga baada ya Simba kutufunga mabao 5-0, kwa kweli niliumia sana kuona tumefungwa idadi kubwa ya mabao, sasa sitagombea tena maana timu inafanya vizuri na pia ni wakati wangu wa kuachia wengine waje kuongoza,” alisema Manji.
Viongozi wengine walioingia madarakani na Manji katika uchaguzi huo mdogo ni Clement Sanga (Makamu Mwenyekiti) aliyejipatia asilimia 62 ya kura.
Wajumbe wa kamati ya utendaji ni Abdallah Bin Kleb, Moses Katabaro, Aaron Nyanda na George Manyama.
Nchunga alilazimika kujiuzulu baada ya wajumbe wake wa kamati ya utendaji kuachia ngazi katika mgogoro huo, hivyo kwa mujibu wa Katiba ya Yanga asingeweza kuendelea kuongoza peke yake.

No comments:

Post a Comment