![]() |
Shabiki wa Yanga akiwa kwenye Uwanja wa Kijitonyama jana, huku amevalia
jezi yenye jina la mchezaji mpya wa timu hiyo, Emmanuel Okwi
anayetarajiwa kuwasili leo kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo. |
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage ameibuka na kusema kuwa lawama za kutokumsajili mshambuliaji wao wa zamani kutoka Uganda, Emmanuel Okwi zielekezwe kwa Kamati ya Usajili na Ufundi wa timu hiyo na wala siyo yeye.
Rage ambaye alikuwa nchini Marekani kwa mwezi
mmoja akimuuguza mwanaye, alisisitiza kuwa Okwi alikwishauzwa kwa timu
ya Etoile Du Sahel ya Tunisia na wala hakuwa wa Simba tena pamoja na wao
kuendelea kudai fedha zao.
Alisema kuwa wakati anakwenda kumuuguza mwanaye,
alikuwa amefanikiwa kusajili wachezaji wawili, Awadh Juma na Badru Ali
tu, lakini huku nyuma bila ya kupata baraka zake, Kamati ya Usajili
ilifanikiwa kumpa mkataba kocha mpya, Zdravko Logarusic kutoka Croatia
na kusajili wachezaji watatu, makipa, Yaw Berko, na Ivo Mapunda na
mlinzi Mkenya, Donald Musoti.
“Ikumbukwe kuwa Okwi alikuwa anakuja mara kwa mara
hapa nchini, lakini kamati hizo hazikuona umuhimu wake, hawakufanya
naye mazungumzo kujua nini kinachoendelea kuhusiana na timu yake ya
Tunisia na sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kutaka kunichafua mimi na
kuonekana mbaya na adui kwa klabu ya Simba,” alisema Rage.
Alisema kuwa kilichokuwa kinazungumzwa muda wote
ni kunitaka mimi kujiuzulu na kuwaachia madaraka, jambo ambalo
haliwezekani kwani lazima wajue kuwa mimi ndiye mkombozi wa Simba.
“Nimefanya mabadiliko makubwa, kuanzia kuongeza
kodi ya mapango yetu na klabu kuingiza fedha, kutoka kodi ya Sh200,000
mpaka sasa ya mamilioni, sasa watu wanataka kuona fedha hizo zinapotea
na kuwatumia watu ili niondoke, nasema hili halitawezekana na kwa
taarifa tu, wale wenye mipango ya kunivamia nyumbani, nimekwisha toa
taarifa polisi na hatua kali watachukuliwa wakithubutu kufanya hivyo,”
alisema.
Alisema kuwa njama nyingi zimefanyika katika suala
la Okwi mpaka kujiunga na Yanga, lakini kwa sasa yeye anasimamia zaidi
suala la malipo ya timu ya Etoile na mchakato huo unakwenda vizuri.
“Hivi leo Mbwana Samatta akijiunga na Yanga au
Azam FC, watanilaumu mimi, Okwi hakuwa mchezaji wetu, wana-Simba wajue
hilo, kuzungumzia suala la Okwi na kunishutumu mimi ni kunionea tu,
walipaswa kujua suala la fedha, nalo nimelizungumza sana na kutoa
ufafanuzi, lakini kwa vile lengo lao mimi niondoke, wanaongea maneno
mengi ya uzushi juu yangu… mimi ni kiongozi mwenye sifa na kujua mambo
ya uongozi, siwezi kukurupuka kujibu suala lolote,” alisema.
Alisema kuwa suala la malipo ya Okwi siyo siri,
kwani Kamati ya Utendaji inaelewa kuwa tumefungua kesi Fifa na kulipa
Dola 10,000 ili malalamiko yetu yapangiwe jaji na kusikilizwa.
“Kuna barua ililetwa na Fifa kwa njia ya DHL,
ilifika klabuni muda mrefu, barua hiyo ilikuwa na majibu ya Fifa na njia
gani tufuate ili tuweze kupata haki yetu ya Dola 300,000 za Marekani,
makusudi haikutiliwa mkazo, leo (jana) nimefanikiwa kulipa Dola 10,000
kutoka mfukoni mwangu na tunasubiri kusikilizwa kwa madai yetu,”
alisema.
No comments:
Post a Comment