
Lunyamila akiwa amelala kitandani hospitalini .PICHA|MAKTABA
HALI ya winga wa zamani wa Yanga na Taifa Stars,
Edibily Lunyamila, inaendelea kuimarika baada ya kuanza kuzungumza kwa
kifupi na watu wanaomtembelea kumjulia hali katika Hospitali ya
Mwanyamala, Dar es Salaam, ambapo amelazwa.
Lunyamila alifikishwa hospitalini hapo Jumatatu ya
wiki hii akitokea nyumbani kwake Mbezi Luis baada ya kuzidiwa
alipopatwa na tatizo la kupumua. Hospitalini hapo alilazimika kufungiwa
mitungi ya gesi ili kumsaidia kupumua.
Jana Jumatano asubuhi Mwanaspoti lilifika
hospitalini hapo na kuweza kusalimiana na Lunyamila kwa kifupi kwani
kutokana na ushauri wa madaktari, nyota huyo wa zamani haruhusiwi
kuzungumza kwa muda mrefu.
“Nashukuru kidogo afadhali,” ndiyo kauli ya Lunyamila kwa mwandishi wa habari hizi aliyetaka kumjulia hali.
Ndugu wa Lunyamila anayemuuguza, Lameck John,
alisema ripoti ya kwanza ya madaktari imesema winga huyo anasumbuliwa na
homa ya matumbo, lakini amechukuliwa vipimo tena kutazama kama ana
matatizo ya moyo.
“Wametuambia anaumwa homa ya matumbo lakini wanatazama pia kujua kama ana matatizo ya moyo,” alisema Lameck.
Juzi Jumanne, baadhi ya viongozi na wanachama wa
Yanga walifika hospitalini hapo na kumhamisha mchezaji huyo kutoka wodi
namba 5B na kumpeleka wodi namba 4 ambako anatibiwa katika mazingira
mazuri zaidi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah
Bin Kleb, mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Mohamed Bhinda na mchezaji wa
zamani wa timu hiyo, Ali Mayayi, ndiyo walioratibu maboresho ya huduma
anayopata Lunyamila hospitalini hapo.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi, naye ni miongoni mwa wadau wa michezo waliojitokeza kumfariji
Lunyamila hospitalini hapo.
Wengine ni Juma Kaseja, Aboubakar Salum ‘Sure Boy’, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, Seleman Matola, Vincent Peter na Idd Moshi.
No comments:
Post a Comment