![]() |
Wachezaji wa Bayern Munich wakishangilia |
ARSENAL imepewa kibarua kizito katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya mtoano baada ya kupangwa kucheza na mabingwa watetezi, Bayern Munich, Februari mwakani.
Bayern inayofundishwa na Pepe Guardiola, kwa sasa
imekuwa katika kiwango cha juu katika misimu mitatu iliyopita ambapo
imefanikiwa kutinga fainali hizo mara mbili mfululizo na kutwaa ubingwa
msimu uliopita katika pambano dhidi ya Borussia Dortmund lililofanyika
mwezi Mei katika Uwanja wa Wembley.
Manchester City ambayo ni mara yao ya kwanza
kufuzu hatua hiyo ya mtoano, imepewa mtihani mzito wa kukabiliana na
Barcelona ambayo itaongozwa na mkali wao, Lionel Messi, ingawa kwa sasa
ni majeruhi.
Manchester United ndio timu ya England iliyopata
nafuu zaidi katika ratiba hii ya hatua ya mtoano na itapepetana na
Olimpiakos ya Ugiriki katika pambano ambalo United inatazamiwa kupita.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Didier
Drogba, anatazamiwa kuwa kivutio katika pambano la mtoano kati ya
Chelsea na Galatasaray baada ya ratiba kuwakutanisha vigogo hao wa
London na Istanbul.
Cristiano Ronaldo ataiongoza Real Madrid kusafiri
mpaka Ujerumani kukipiga na Schalke 04 wakati staa wa kimataifa wa
Sweden, Zlatan Ibrahimovic, naye atafunga mkanda na timu yake PSG kwenda
huko huko Ujerumani kuchuana na Bayer Leverkusen.
AC Milan baada ya kupita katika kundi lao
wakishika nafasi ya pili nyuma ya Barcelona, nao wamepewa zawadi ya
kwenda tena Hispania kukipiga na Atletico Madrid katika pambano
linalotarajiwa kuwa kali na la kusisimua.
Wanafainali wa msimu uliopita, Borussia Dortmund
wamepewa kibarua cha kwenda Ulaya Mashariki kukipiga na Zenit Petersburg
ambayo inaongozwa na staa wa zamani wa Arsenal, Andrey Arshavin.
Timu zote zilizomaliza nafasi ya pili zitaanza
kucheza mechi zake katika viwanja vya nyumbani na mechi za kwanza
zitachezwa kati ya Februari 18/19 na Februari 25/26, wakati zile za
marudiano zitachezwa kati ya Machi 11/12 na Machi 18/19.
Mwanasport.
Mwanasport.
No comments:
Post a Comment