![]() |
Straike wa zamani wa Manchester United,Andy Cole. |
STRAIKA wa zamani wa Manchester United,Andy Cole amesema Tanzania ina vipaji vingi vya soka lakini kinachowakwamisha kucheza soka la kulipwa Ulaya ni miundombinu ya kuwatoa katika hatua moja kwenda nyingine.
Cole aliiambia Mwanaspoti kuwa,Tanzania ni
miongoni mwa nchi zilizojaliwa kuwa na vijana wenye vipaji vya hali ya
juu lakini wanakumbana na changamoto ya mahala wanapoweza kuonyesha
vipaji vyao.
Alisema vijana wengi hapa nchini wana uwezo mzuri
wa soka ambao unawawezesha kucheza popote duniani isipokuwa hawapati
nafasi ya kuonyesha vipaji walivyonavyo na hata wakipata muda unakuwa
umekwisha.
“Ninavyojua Tanzania ina vijana wengi wenye vipaji
vya kucheza soka la kulipwa popote duniani ikiwemo Ulaya, nadhani
tatizo ni mahali ambapo wanaweza kuonyesha vipaji vyao ili wengine
wawachukue,” alisema Cole ambaye alitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya
akiwa Man United mwaka 1999.
Alisema vijana wanatakiwa kujiingiza katika soka
la kulipwa wakiwa na umri mdogo kwani hapo wanaweza kupata muda wa
kujifunza zaidi kuhusu soka la kisasa.
“Naona mwanga kwamba ipo siku Tanzania itatoa
wachezaji wa kulipwa watakaocheza soka la kulipwa England au Ulaya,”
alisema Cole ambaye aliwahi pia kuichezea timu za Arsenal, Newcastle na
Manchester City.
Cole alikuwepo nchini katika kampeni maalum ya Mimi ni bingwa yenye lengo la kuhamasisha soka Tanzania.
Hii ni mara ya pili kwa Cole kutua nchini baada ya
kufanya hivyo mwaka jana alipokuja katika michuano ya kuibua vipaji vya
vijana ya Airtel Rising Star.
Wachezaji kadhaa wa Tanzania wakiwemo Henry Joseph
wa Simba,Nizar Khalfan na Mrisho Ngassa wa Yanga wamewahi kupata nafasi
ya kucheza nje ya nchi lakini hawakuweza kucheza katika ligi kubwa kama
ya England hata daraja la tatu.
Nizar amewahi kucheza soka la kulipwa nchini
Canada katika klabu ya Vancouver Whitecaps kabla ya mwaka jana kurejea
nchini, wakati Joseph amewahi kucheza Kongvinger ya Norway na mwaka huu
akarudi nyumbani.
Ngassa alipata nafasi ya kufanya majaribio katika klabu ya West Ham lakini hakufuzu.
No comments:
Post a Comment