Sunday, 15 December 2013

ROONEY MWANASOKA MWENYE PESA NDEFU ZAIDI UINGEREZA


TIMU yake ya Manchester United inagaragara kwenye nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu England, lakini straika Wayne Rooney anashika namba moja kwa wanasoka raia wa Uingereza wanaotesa kwa utajiri katika ligi hiyo.
Kwenye orodha ya wanasoka 10 matajiri, mastaa Rio Ferdinand, Frank Lampard, John Terry na Steven Gerrard wameingia ndani ya tano bora, huku jina la staa wa West Ham United, Joe Cole likiwaduwaza wengi kutokana na kuwamo kwenye orodha hiyo.
Wazawa wengine wenye pesa za nguvu kwenye Ligi Kuu England ni Ashley Cole, Michael Carrick na Ashley Young, huku James Milner akiwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi mwenye pesa kwa kuwa na umri wa miaka 27.
Rooney anavyofunika
Akiwa na umri wa miaka 28, supastaa huyo wa England soka lake limemfanya kuingiza pesa za nguvu na kuwaacha kwa mbali Waingereza wenzake kwenye orodha hiyo.
Akiaminika kuwa na kipato kinachofikia Pauni 45 milioni, Rooney anapokea mshahara unaokadiriwa Pauni 250,000 kwa wiki na kumiliki mikataba minono ya kibiashara ukiwamo wa kampuni ya Nike.
Kitokana na kipato chake, Rooney anamzidi mtu anayeshika nafasi ya pili, Rio Ferdinand kwa tofauti ya Pauni 8 milioni kutokana na beki huyo wa kati wa Manchester United kumiliki Pauni 37 milioni.
Rio anavuna pesa kupitia mgahawa
Kwa wanasoka Waingereza wenye pesa na wanaoendelea kung’ara kwenye soka, Ferdinand anatajwa kuwa na kipato cha kinachofikia Pauni 37 milioni, ambazo amekipata kupitia mshahara wake anaolipwa Manchester United na biashara yake ya mgahawa pamoja na jarida.
Staa huyo anamiliki mgahawa wake unaoitwa Rosso uliopo jijini Manchester unamfanya apige pesa nyingi zaidi ukiweka kando kipato kingine anachokiingiza kutokana na jarida lake la #5.
Kuwekeza kwenye miradi ya biashara ni kitu kinachomfanya Rio kupiga pesa za maana licha ya sasa soka lake kuelekea ukingoni kutokana na kuwa na umri wa miaka 35.

No comments:

Post a Comment