![]() |
Kikosi cha Simba. |
SIMBA imeichapa KMKM ya Zanzibar mabao 3-1 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa jana Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo ambayo ilikuwa ya kwanza kwa
kocha mpya wa kikosi hicho, Zdravko Logarusic ambaye alianza kwa staili
ya kuwahamisha namba baadhi ya wachezaji.
Kocha huyo raia wa Crotia alimpanga Issa Rashid
‘Baba Ubaya’ kucheza kama winga wa kushoto badala ya beki wa kushoto
nafasi aliyokuwa akicheza siku zote na kumuanzisha Henry Joseph kama
beki wa kati akicheza sambamba na Joseph Owino.
Henry alipangwa nafasi hiyo kutokana na uhaba wa
mabeki wa kati baada ya Gilbert Kaze kuwa kwao Burundi akiwa mgonjwa wa
kifua ingawa Simba tayari imemsajili beki mpya kutoka Gor Mahia ya Kenya
Donald Musoti.
Katika mchezo huo ambao haukuhudhuriwa na
mashabiki wengi, Logarusic pia alimuanzisha kipa wake mpya, Yaw Berko
kwa mara ya kwanza huku timu hiyo ikitawala vyema kwenye safu ya kiungo
ambayo iliongozwa na Jonas Mkude na Said Ndemla waliofunika katika
nafasi hiyo.
Said Ndemla ndiye aliyeanza kuamsha shangwe kwa
mashabiki wa Simba baada ya kufunga bao dakika ya 11 kwa shuti kali
lililomshinda kipa wa KMKM, Mudathir Khamis kabla ya Edward Christopher
kufunga la pili dakika ya 16.
Hata hivyo Simba walionekana kupwaya kipindi cha
pili na kuwaruhusu KMKM kufunga bao la kwanza dakika ya 73 likifungwa na
mchezaji wa zamani wa Simba, Alli Shiboli kwa penalti baada ya beki
Omary Salum kumchezea rafu mshambuliaji huyo.
Hata hivyo wakati mashabiki wakidhani matokeo
yatabaki hivyo Henry Joseph aliwainua tena mashabiki wa Simba vitini kwa
kufunga bao la tatu kwa penalti dakika ya 88 baada ya Issa Abdallah
kufanyiwa madhambi na beki Khamis Ally wa KMKM katika eneo la penalti.
Kikosi Simba: Berko, Haruna Shamte, Omary Salum,
Henry Joseph, Joseph Owino,Jonas Mkude,Edward Christopher/William
Lucian, Said Ndemla/Miraji Adam,Betram Mwombeki/Amiss Tambwe, Uhuru
Seleman na Issa Rashid.
No comments:
Post a Comment